Jeshi la Lebanon: Vitisho vya Israel havitutishi
Kamanda wa Jeshi la Lebanon ametangaza kuwa jeshi la nchi hiyo liko tayari kukabiliana na aina yoyote ya vitisho vya jeshi la utawala haramu wa Israel.
Joseph Aoun ameyasema hayo wakati alipokagua vikosi vya jeshi la Lebanon vilivyopo katika mipaka ya eneo la kusini mwa Lebanon na kuongeza kuwa, vitisho vinavyoendelea kutolewa na utawala haramu wa Israel dhidi ya taifa la Lebanon haviwezi kulifanya jeshi la nchi hiyo kuuogopa utawala huo khabithi na kinyume chake, litaendelea kutekeleza wadhifa wake wa kuitetea ardhi yote ya nchi hiyo.
Aoun amesisitiza kuwa, ushindi wa jeshi la Lebanon katika operesheni za 'Fajrul-Jurud' katika vita na magaidi umerejesha amani na usalama ndani ya nchi na kuwa na taathira chanya kwa Lebanon.
Kwa mara kadhaa ndege za kivita na zile za upelelezi za utawala haramu wa Israel zimekuwa zikikiuka haki ya kujitawala ya Lebanon na kuingia katika anga ya nchi hiyo. Kutokana na chokochoko hizo, jeshi la Lebnon limewasilisha ripoti kwa askari wa Umoja wa Mataifa walioko nchini humo, UNIFIL.
Azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililotolewa baada ya vita vya siku 33 kati ya harakati ya Hizbullah na Israel mwaka 2006 liliutaka utawala huo bandia kukomesha chokochoko zake dhidi ya Lebanon. Hata hivyo utawala huo khabithi umekuwa ukikiuka azimio hilo kwa kuingia katika maji na anga ya nchi hiyo.