Algeria yataka kurejea Syria katika Jumuiya ya Kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa uhusiano wa nchi hiyo na Syria ni wa kihistoria na kusisitiza kuwa Algeria inataka Syria irejee katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League).
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Arab League mwezi Novemba mwaka 2011 baada ya kuanza mgogoro huko Syria walisimamisha unachama wa nchi hiyo ndani ya Jumuiya ya Kiarabu. Mgogoro ulioanza huko Syria tangu mwaka 2011 kufuatia hujuma kubwa za makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wake ikiwemo Uturuki lengo likiwa ni kubadili mlingano katika eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni.
Abdulqadir Masahil jana alitilia mkazo pia udharura wa kupatiwa ufumbuzi hitilafu zote katika Mashariki ya Kati ukiwemo mgogoro uliojitokeza kati ya Saudi Arabia na waitifaki wake pamoja na Qatar. Saudi Arabia na waitifaki wake yaani Misri, Imarati na Bahrain zimekata uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar tangu tarehe 5 Juni mwaka huu kwa madai kwamba Doha haiendi sambamba na mrengo wa nchi za Kiarabu zinazoongozwa na Riyadh; na mbali na kuiwekea Qatar vikwazo, nchi hizo nne pia zimeifungia Qatar mipaka ya nchi kavu, baharini na anga.