UN: Kura ya maoni ya kujitenga Kurdistan kutoka Iraq itavuruga amani
Kwa mara nyingine tena António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu kitendo cha viongozi wa eneo la Kurdistan huko kaskzini mwa Iraq kushikilia suala la kufanyika kura ya maoni ya kujitenga eneo hilo na serikali kuu ya nchi hiyo.
Stéphane Dujarric, Msemaji wa Guterres amesema Katibu Mkuu wa UN amesikitishwa na kura hiyo ya maoni na kusisitiza kuwa, haitakuwa na tija nyingine ghairi ya kuzidisha ukosefu wa amani sio tu kwa Iraq, bali katika eneo lote la Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq amesema serikali ya Baghdad haitatilia maanani matokeo ya kura hiyo ya maoni iliyofanyika jana Jumatatu.
Amesisitiza kuwa, zoezi hilo limefanyika kinyume cha sheria na bila baraka na uungaji mkono wa taifa la Iraq na jamii ya kimataifa.
Alkhamisi iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio lililopinga suala la kuitishwa kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq.
Mbali na Umoja wa Mataifa, kura hiyo ya maoni imepingwa vikali na serikali kuu ya Iraq, makundi mbalimbali ya kisiasa nchini humo na nchi karibu zote za Mashariki ya Kati zikiwemo Iran na Uturuki.
Matokeo rasmi ya kura hiyo ya maoni yanapaswa kutolewa chini ya masaa 72 baada ya vituo vya kupigia kura kufungwa (saa 12 jioni kwa saa za Iraq hapo jana).