Saudia yaendeleza njama dhidi ya makundi yanayopambana na Israel
Jumuiya ya vyama vya siasa nchini Lebanon umetangaza kuwa, matamshi yaliyotolewa na Waziri Mshauri katika Masuala ya Ghuba ya Uajemi wa Saudi Arabia kuhusu harakati ya Hizbullah ya Lebanon yanaakisi siasa za utawala wa kifalme wa nchi hiyo dhidi ya kambi inayopambana na utawala haramu wa Isarel.
Jumuiya hiyo inayojulikana kwa jina la Liqaaul Ahzab Ahzab imesema kuwa, wito uliotolewa na Thamer Al-Sabhan wa kuundwa eti muungano wa kukabiliana na Hizbullah na kupongeza vikwazo dhidi ya harakati hiyo unaonesha msimamo wa kihasama wa Saudi Arabia.
Liqaaul Ahzab imeongeza kuwa, msimamo huo wa Saudia unaonesha kuwa, watawala wa nchi hiyo wanaendelea kula njama dhidi ya harakati ya Hizbullah ili kuzuia ushawishi wa harakati hiyo na washirika wake na kwamba sera na siasa hizo zinahudumia malengo na maslahi ya kikoloni ya Marekani na Israel.
Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa, uharibifu huo wa watawala wa Saudi Arabia dhidi ya Hizbullah na harakati za mapambano ni mwendelezo wa siasa za kusambaza zaidi fikra za kigaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia.