Walowezi wa Kizayuni wauhujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni leo wameuhujumu Msikiti wa Al Aqsa na kuvunjia heshima eneo hilo takatifu la Kiislamu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Palestina, walowezi wa Kizayuni wapatao 74, wakiwa wanalindwa na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel, wametumia Mlango wa Maghariba kuuhujumu Msikiti wa al Aqsa.
Wazayuni wamekuwa wakitekeleza hujuma kama hizo za kuuvunjia heshima msikiti mtukufu wa al-Aqsa kwa himaya ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, Masjidul Aqswa ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kituo cha mwanzo cha safari ya Mi'iraji ya Mtume Mtukufu SAW, lakini umekuwa ukishambuliwa na kuvunjiwa heshima na magenge ya Kizayuni yenye misimamo mikali huku yakipata uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni.
Wapigania ukombozi wa Palestina wanasisitiza kuwa, Quds ndio mji mkuu wa dola huru la Palestina litakaloundwa katika mustakabali.