Naibu Mkuu wa HAMAS: Israel ndio "Hatari Kuu"
(last modified Thu, 26 Oct 2017 15:16:41 GMT )
Oct 26, 2017 15:16 UTC
  • Naibu Mkuu wa HAMAS: Israel ndio

Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amezitaka nchi na pande zote za eneo la Mashariki ya Kati zikubaliane na fikra kwamba utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ndio "Hatari Kuu".

Saleh al-Arouri ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Aljazeera ya Qatar na kuongeza kuwa: kuikubali fikra hiyo  kuhusu Israel kwamba ndio hatari kuu ndilo jambo linalohitajiwa kwa ajili ya kuunga mkono muqawama na kukidhi mahitaji uliyonayo.

Saleh al-Arouri ameeleza bayana kwamba Hamas inaamini "silaha" ni kitu chenye "wajibu wa lazima kuwepo" na wala hakina mgongano na maridhiano ya kitaifa yaliyofikiwa baina yake na harakati ya Fat'h na kwamba madamu ukaliaji ardhi za Palestina kwa mabavu ungali unaendelea, silaha nazo pia lazima ziendelee kuwepo.

Wanamuqawama wa Izzuddin al Qassam, tawi la kijeshi la Hamas

Naibu Mkuu wa Hamas ameeleza pia kwamba kwa mtazamo wa harakati hiyo mkataba wa maridhiano ya kitaifa ni kipaumbele kisichoweza kubadilika, hata hivyo mbali na kuyakataa masharti ya Israel kuhusiana na maridhiano hayo amesisitiza pia kuwa: Hamas haitoitambua rasmi Israel.

Baraza la usalama la utawala wa Kizayuni wa Israel limetangaza kuwa utawala huo utafanya mazungumzo na Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa sharti kwamba harakati ya muqawama ya Hamas ipokonywe silaha.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya harakati za Fat'h na Hamas, kuanzia tarehe Mosi Desemba mwaka huu, serikali ya umoja wa kitaifa ya Palestina itakuwa na mamlaka ya kuendesha masuala ya eneo la Ukanda wa Gaza kama inavyofanya katika eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.../ 

Tags