Ndege za kivita za Saudia zaendelea kuua raia nchini Yemen
Raia wasipungua saba Wayemen wamepoteza maisha yao baada ya ndege za kivita za Saudi Arabia kuvurumisha mabomu katika mkoa wa Sa'ada kaskazini mashariki mwa nchi hiyo siku chache tu baada ya jinai sawa na hiyo.
Kwa mujibu wa Televisheni ya Al-Masirah, katika jinai hiyo ya Ijumaa, ndege za kivita za Saudia zilivurumisha mabomu katika majengo kadhaa ya raia katika mji wa mpakani wa Baqim na kupelekea raia kadhaa kuuawa wakiwemo wanawake na watoto.
Hujuma hiyo imekuja siku chache tu baada ya ndege za kivita za Saudia kudondosha mabomu katika maeneo ya raia, likiwemo soko, mkoani Sa'ada na kupelekea raia 29 kuuawa.
Vita vya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen vilianzishwa mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abd Rabbuh Mansur Hadi.
Vita hivyo vingali vinaendelea kwa mwaka wa tatu sasa bila ya utawala wa Aal Saud na waitifaki wake kufikia malengo haramu waliyokusudia. Watu zaidi ya 13,000 , wengi wakiwa ni wanawake na watoto, wameuawa katika hujuma ya Saudia nchini Yemen.
Mwezi uliopita Umoja wa Mataifa uliiorodhesha Saudia miongoni mwa nchi zinazoua watoto kiholela vitani. Katika orodha hiyo iliyotangazwa Oktoba 5 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, muungano unaoongozwa na Saudia katika vita dhidi ya Yemen umetajwa kuwa muuaji mkubwa wa watoto.