Nov 04, 2017 07:35 UTC
  • Ngome ya mwisho ya Daesh Iraq yadhibitiwa, al-Abad atoa pongezi

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abad ametoa pongezi kufuatia kukombolewa eneo la al-Qaim, magharibi mwa mkoa wa al-Anbar kutoka mikononi mwa wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh.

Sambamba na kutoa pongezi hizo, Al-Abad ametangaza kuwa, kukombolewa eneo hilo na jeshi la serikali na katika kipindi kifupi sana, kunadhihirisha uwezo mkubwa wa nchi hiyo katika kukabiliana na makundi ya kigaidi na maadui wa taifa la Iraq. Jioni ya jana Abdul-Amir Rashid Yarullah, kamanda wa jeshi la Iraq sambamba na kutangaza habari hiyo, alisema kuwa mji wa mpakani wa al-Qaim wa mkoa wa al-Anbar, ulikuwa ngome muhimu sana kwa kundi la Daesh lakini sasa umedhibitiwa na jeshi la serikali.

Baadhi ya askari wa Iraq wanaoshiriki operesheni dhidi ya ugaidi

Operesheni ya kukombolewa magharibi mwa mji wa al-Anbar kupitia jeshi la serikali na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi, ilianza tarehe 26 Oktoba mwaka huu. Kukombolewa mji huo muhimu kumezifanya siku za uhai wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq kuhesabiwa ambapo jeshi la nchi hiyo limesema kuwa hivi karibuni kutatolewa habari ya ushindi kamili dhidi ya kundi hilo. Aidha kudhibitiwa mji huo kumewafanya askari wa Iraq na Syria kukutana katika mpaka wa pamoja na hivyo kutoa pigo kwa magaidi hao wa Kiwahabi.

Tags