UN: Yemen inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa duniani
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu hatua ya Saudi Arabia na washirika wake ya kufunga kabisa mipaka ya Yemen kwa siku ya tano mfululizo na kusisitiza kuwa Yemen inakabiliwa na baa kubwa zaidi la njaa duniani katika miongo ya hivi karibuni.
Stéphane Dujarric amesema kuwa, ili kuweza kuzuia baa hilo la njaa, Saudia na washirika wake wanapaswa kukomesha mzingiro na kufungua mipaka ya anga, nchi kavu na majini ya Yemen. Vilevile ametoa wito wa kuanzishwa tena huduma za anga za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada ya kibinadamu kuelekea San'aa na Aden.
Saudi Arabia na washirika wake Jumapili iliyopita walifunga kikamilifu njia zote za nchi kavu, baharini na angani za kuingia Yemen baada ya jeshi la nchi hiyo kujibu jinai za Saudia kwa kuvurumusha makombora dhidi ya uwanja wa ndege wa Mfalme Khalid katika mji mkuu wa nchi hiyo Riyadh.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imetangaza kuwa hatua hiyo ya Saudi Arabia ni dalili ya kushindwa na kuchanganyikiwa viongozi wa kisiasa na kijeshi wa utawala wa kifalme wa Saudia.

Saudi Arabia ikishirikiana na Marekani, Israel na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zilianzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya Yemen Machi mwaka 2015. Maelfu ya raia wasio na hatia wameuawa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi hayo.