Rais wa Lebanon: Matamshi ya Saad Hariri hayana itibari
Rais Michel Aoun wa Lebanon amesema: Saad Hariri, tangu siku ya Jumamosi hadi sasa yuko nchini Saudi Arabia katika mazingira tata na yasiyoeleweka; na misimamo yake ni misimamo ya kutia shaka na kutatanisha.
Mnamo tarehe 4 Novemba, Saad Hariri alitangaza kujiuzulu wadhifa wa uwaziri mkuu wa Lebanon kupitia taarifa aliyosoma akiwa mjini Riyadh, Saudi Arabia. Hata hivyo rais wa Lebanon amesema, kujiuzulu kwa Hariri si halali kisheria.
Katika taarifa aliyotoa jana usiku Rais Michel Aoun amesisitiza kuwa haiwezekani kuyaamini maneno aliyosema Saad Hariri akiwa Saudi Arabia na kuyachukulia kuwa ni yenye itibari.
Michel Aoun amebainisha kuwa Hariri yuko huko Riyadh katika mazingira ambayo hawezi kuzungumza kwa uhuru na kwamba waziri mkuu huyo wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu amewekewa masharti kuhusu ukaazi wake ndani ya Saudia na hata juu ya namna ya kuwasiliana na familia yake.
Katika mahojiano ya mwanzo kurushwa hewani tangu alipotangaza kujiuzulu uwaziri mkuu ambayo alifanya na kanali ya televisheni ya Al-Mustaqbal jana usiku, Saad Hariri hakuashiria chochote kuhusu kimya cha wiki nzima alichoonyesha wala sababu ya kuichagua Saudia kuwa makaazi yake baada ya kutangaza kujiuzulu, na badala yake akadai kuwa alichukua uamuzi wa kujiuzulu baada ya kuongezeka vitisho vya kiusalama dhidi yake na Lebanon.
Kanali nyingi za televisheni za Lebanon ikiwemo televisheni ya taifa zilitangaza jana jioni kwamba kutokana na kuwepo katika mazingira ya kutatanisha, hazitorusha hewani mahojiano aliyofanyiwa Hariri na kanali ya Al-Mustaqbal na kwamba maelezo aliyotoa kwenye mahojiano hayo hayana itibari.../