Iran yasisitiza haingilii mambo ya ndani ya nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36374-iran_yasisitiza_haingilii_mambo_ya_ndani_ya_nchi_nyingine
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Sera ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutoingilia kamwe masuala ya ndani ya nchi nyingine."
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Nov 13, 2017 12:04 UTC
  • Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Sera ya kimsingi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kutoingilia kamwe masuala ya ndani ya nchi nyingine."

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari na kuongeza kuwa, Iran daima inataka amani na utulivi nchini Lebanon. Amesema kadhia ya kujiuzulu Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri inawahusu Walebanon wenyewe.

Akijibu swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusu ombi la Saudia la kuitishwa kikao cha dharura cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu dhidi ya Iran, Qassemi amesema: "Si mara ya kwanza Saudia kuchukua hatua kama hiyo. Wakuu wa Saudia, kutokana na matatizo ya ndani na nje ya nchi hiyo, na pia kutokana na kushindwa mfululizo katika medani kadhaa,  sasa wanajaribu kushinikiza kuwepo kauli moja dhidi ya Iran."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema matukio ya wiki moja iliyopita yanaonyesha kufeli sera za Saudia katika eneo na kuongeza kuwa: "Kikao kijacho cha Jumuiya Nchi za Kiarabu mjini Cairo hakitakuwa na matokeo mazuri kwa Saudia kwani nchi za eneo hili nazo pia zinafuatilia kwa karibu yanayojiri."

Qassemi pia ameashiria uchochezi wa Saudia katika kuzusha vita vya niaba nchini Lebanon na kusema: "Iran inahimiza kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na inahimiza kufanyika mazungumzo."

Rafiq Hariri akitangaza kujiuzulu kama Waziri Mkuu wa Lebanon

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje pia amesema kunafanyika mashariano kuhusu safari tarajiwa nchini Iran ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa huku akiongeza kuwa tarehe  ya safari hiyo bado haijulikani. Aidha Qassemi amekosoa msimamo wa Macron kuhusu mpango wa makombora ya kujihami ya Iran. Amesema Rais wa Ufaransa ametoa matamshi pasina kutathmini hali ya mambo na hivyo amewataka wakuu wa Ufaransa kuwa waangalifu kuhusiana na masuala ya eneo ili wasivuruge uhusiano wa pande mbili. Kuhusiana na kuendelea kuwepo Iran nchini Syria baada ya kuangamizwa kundi la kigaidi la ISIS, Qassemi amesema: "Hatua ya Iran ya kuweko nchini Syria kunatokana na mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo, na baada ya kuangamizwa kikamilifu ISIS , Iran itaendelea kuwa tayari kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili."