Qatar: Saudia inayakandamiza 'mataifa madogo' kwa lengo la kuyapigisha magoti
(last modified Sat, 18 Nov 2017 07:35:47 GMT )
Nov 18, 2017 07:35 UTC
  • Qatar: Saudia inayakandamiza 'mataifa madogo' kwa lengo la kuyapigisha magoti

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema utawala wa Saudi Arabia unachochea migogoro na mivutano katika eneo la Mashariki ya Kati sambamba na kuzikandamiza na kuzinyanyasa nchi ndogo katika eneo ili kuzishinikiza zipige magoti mbele yake.

Mohammed bin Abdulrahman Aal-Thani aliyasema hayo jana Ijumaa katika kikao na waandishi wa habari mjini Washington na kufafanua kuwa, karata mpya ya kisiasa ya Riyadh dhidi ya Lebanon inafanana na msimamo wa utawala wa Aal-Saud dhidi ya Doha.

Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni mwaka huu, Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain ziliiwekea Qatar vikwazo vya kila upande vya angani, majini na ardhini na kuyafukuza mashirika na raia wa nchi hiyo katika nchi hizo kwa tuhuma kwamba Doha inaunga mkono ugaidi na haiko tayari kukata uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kuimarika uhusiano wa Saudia na Israel kunaenda sambamba na kumeguka uhusiano wa Riyadh na nchi za Kiarabu

Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Qatar amesema Doha ipo tayari kwenda kwenye meza ya mazungumzo kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Hii ni katika hali ambayo, wiki iliyopita, Abdulrahman Aal-Thani alisema katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya TRT ya Uturuki kwamba, uhusiano wa Qatar na Iran ni mzuri na hauwezi kuvurugwa na mashinikizo ya Saudi Arabia.

Alisema nchi zilizoiwekea vikwazo Qatar hadi hivi sasa zinaendeleza ugomvi na zinapinga kufanyika mazungumzo, bali zinatumia njia zisizo sahihi kufanikisha malengo yao. 

 

Tags