Hamas: Huenda Trump akaitambua Israel kama dola la Kiyahudi
(last modified Sun, 24 Dec 2017 08:04:35 GMT )
Dec 24, 2017 08:04 UTC
  • Hamas: Huenda Trump akaitambua Israel kama dola la Kiyahudi

Kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, Ismail Haniya amesema amepokea taarifa za siri kuwa Washington inapanga kuutambua utawala haramu wa Israel kama dola la Kiyahudi.

Akiongea mjini Gaza hapo jana, Haniya amesema lengo la Rais Donald Trump wa Marekani kuazimia kuchukua hatua hiyo ni kutoa kibali kwa Israel kushadidisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina sambamba na kubatilisha haki ya Wapalestina ya kurejea katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu.

Kadhalika Haniya ambaye ni Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Hamas amesisitiza kuwa, kuna udharura kwa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuangalia upya sera zake na kutoa msimamo madhubuti dhidi ya Israel na Marekani.

Rais Donald Trump wa Marekani

Amesisitiza kuwa, Quds ni mji mkuu wa kimaanawi na kisiasa wa taifa la Palestina na Waislamu wote duniani na kwamba njama zozote za kuuyahudisha zitagonga mwamba.

Disemba 6 Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa eti Quds ni mji mkuu wa utawala haramu wa Israel, hatua ambayo imepingwa na kulaaniwa vikali na aghlabu ya nchi duniani na taasisi za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags