Mahmoud Abbas: Wapalestina watabaki katika ardhi yao mpaka Palestina ikombolewe
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesisitiza kwamba: Wapalestina wataendelea kubaki katika aradhi yao hadi Palestina itakapokombolewa.
Mahmoud Abbas ametoa sisitizo hilo pamoja na kutangaza kwamba Quds ni mji mkuu wa milele wa watu wa Palestina na kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kuisimamisha Intifadha ya wananchi wa Palestina.
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameeleza bayana kwamba: vyovyote vile utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake watakavyotaka kuibadilisha historia, Wapalestina hawatohama katika ardhi yao.
Katika upande mwengine, Nabil Sha'ath, mshauri wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema: Marekani ilikuwa ikijiona kuwa ndiye mpatanishi pekee kati ya Wapalestina na Waisraeli, lakini ukweli ni kwamba nchi hiyo katu haijawa mpatanishi, si kwa mtazamo wa kiusalama wala kwa mtazamo wa kuwa na uwazi.
Sha'ath amesisitiza kwamba harakati na juhudi za kukabiliana na mpango wa Wazayuni kwa njia ya kupigania kutambuliwa rasmi nchi ya Palestina katika uga wa kimataifa zingali zinaendelea.../