Netanyahu: Makao ya Bunge na Serikali ya Israel yatakuwa Baitul Muqaddas
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amesema makao ya bunge na serikali ya utawala huo haramu yatahamishiwa mji wa Baitul Muqaddas.
Akizungumza katika mkutano wa kila mwaka na waandishi wa habari wa nje, Benjamin Netanyahu aidha amesisitiza kuwa hatofanya mazungumzo yoyote na Wapalestina kuhusiana na Quds tukufu.
Waziri Mkuu huyo wa utawala haramu wa Kizayuni aidha amedai kwamba Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ndiye mtu anayekwamisha mchakato wa mazungumzo ya mapatano.
Itakumbukwa kuwa tarehe 6 ya mwezi uliopita wa Desemba 2017, Rais Donald Trump wa Marekani aliitangaza Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel. Trump aidha alieleza azma yake ya kuuhamishia kwenye mji huo ubalozi wa Marekani ulioko Tel Aviv suala ambalo liliamsha hasira kubwa za wananchi wa Palestina na kulaaniwa pia kimataifa.
Katika jibu yaliyotoa kwa hatua hiyo ya Trump, makundi mbalimbali ya muqawama ya Palestina yalitangaza kuwa uamuzi huo utakuwa na matokeo mabaya kwa Israel na bila ya shaka utasababisha kuibuka Intifadha nyengine dhidi ya utawala huo wa Kizayuni.
Mnamo tarehe 21 Desemba, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio lililoungwa mkono na nchi 128 wanachama na kupingwa na nchi tisa tu huku 35 nyengine zikiamua kutopiga kura. Kwa mujibu wa azimio hilo, Umoja wa Mataifa hautoitambua Baitul Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.../