Utawala wa Kizayuni wa Israel waiomba radhi rasmi Jordan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i39171-utawala_wa_kizayuni_wa_israel_waiomba_radhi_rasmi_jordan
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeiomba radhi rasmi Jordan kutokana na tukio lililojiri mwaka uliopita la kuuliwa raia wawili wa Jordan na afisa wa jeshi wa Kizayuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 19, 2018 03:54 UTC
  • Utawala wa Kizayuni wa Israel waiomba radhi rasmi Jordan

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeiomba radhi rasmi Jordan kutokana na tukio lililojiri mwaka uliopita la kuuliwa raia wawili wa Jordan na afisa wa jeshi wa Kizayuni.

Utawala wa Kizayuni jana ulioomba radhi rasmi Jordan kutokana na tukio la mwezi Julai mwaka 2017 lililotokea kwenye ubalozi wa utawala huo haramu mjini Amman ambapo afisa wa jeshi wa Kizayuni wa ubalozi huo aliwaua kwa kuwapiga risasi raia wawili wa Jordan na vilevile kutokana na mauaji ya mwaka 2014 ya Raed Zeiter, jaji Mpalestina aliyekuwa akifanya kazi nchini Jordan ambaye aliuliwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mazishi ya Raed Ziter

Muhammd Al-Muumini, Waziri wa Habari na msemaji wa serikali ya Jordan ametangaza kuwa baada ya kupita miezi sita, utawala wa Kizayuni umetuma taarifa ya kueleza masikitiko na kuomba radhi rasmi kuhusiana na tukio la ubalozini.

Al-Muumini aidha ameongeza kuwa, Israel imekubali kutekeleza masharti yote yaliyotolewa na Jordan kuhusu ufuatiliaji wa hatua za kisheria kuhusiana na tukio la ubalozi wa utawala huo mjini Amman.

Sambamba na hatua hiyo, ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni imetangaza kuwa ubalozi wa Israel nchini Jordan utaanza tena shughuli zake hivi karibuni.

Tarehe 23 Julai mwaka 2017 raia wawili wa Jordan waliuliwa kwa kupigwa risasi na askari wa utawala wa Kizayuni katika ubalozi wa utawala huo mjini Amman. Kufuatia tukio hilo, balozi wa Israel pamoja na wafanyakazi wa ubalozi walilazimika kuondoka nchini Jordan.../