Waziri Mkuu wa Iraq azungumza na Barzani kuhusu Kurdistan ya Iraq
(last modified Sun, 21 Jan 2018 03:09:33 GMT )
Jan 21, 2018 03:09 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq azungumza na Barzani kuhusu Kurdistan ya Iraq

Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi na Nechirvan Barzani, rais wa utawala wa ndani wa eneo la Kurdistan la Iraq wamefanya mazungumzo kuhusiana na matukio ya hivi karibuni na mgogoro uliozuka baina ya Baghdad na Erbil baada ya Kurdistan kuitisha kura ya maoni ya kujitenga na Iraq.

Vyombo vya habari vya Iraq vimeripoti kuwa, baada ya kupita takriban miezi minne ya kukatika uhusiano wa kidiplomasia na kisiasa kati ya Erbil na Baghdad, hii ni mara ya kwa rais wa serikali ya ndani ya Kurdistan ya Iraq, kutembelea Baghdad.

Mgogoro baina ya Erbil na Baghdad ulizushwa na kura ya maoni iliyoitishwa na Masoud Barzani, rais wa zamani wa serikali ya ndani ya eneo la Kurdistan la Iraq ambaye aliitisha kura hiyo ya maoni tarehe 25 Septemba mwaka jana licha ya kupingwa vikali ndani na nje ya Iraq. Serikali ya Baghdad ilikihesabu kitendo hicho kuwa ni kinyume na katiba ya Iraq na kinakinzana na wajibu wa kulindwa umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Nechirvan Barzani, rais wa utawala wa ndani wa eneo la Kurdistan la Iraq

 

Mbali na Baghdad, majirani wa Iraq na taasisi za kimataifa kama vile Umoja wa Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa nazo zilipinga kura hiyo ya maoni.

Serikali ya Baghdad iliweka masharti kadhaa kama utangulizi wa kufanya mazungumzo na Erbil ikiwa ni pamoja na kufutwa kabisa matokeo ya kura hiyo haramu ya maoni sambamba na vivuko vyote vya mpaka na viwanja vya ndege kuwa chini ya serikali kuu kama ambavyo mapato yote ya mafuta na yasiyo ya mafuta yakiwemo pia mapato ya ushuru na kodi yasimamiwe moja kwa moja na serikali kuu ya Baghdad.