HAMAS yasisitiza kuimarisha uhusiano wake na Iran na Hizbullah ya Lebanon
(last modified Sun, 21 Jan 2018 14:10:15 GMT )
Jan 21, 2018 14:10 UTC
  • HAMAS yasisitiza kuimarisha uhusiano wake na Iran na Hizbullah ya Lebanon

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema uhusiano wa harakati hiyo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati ya Hizbullah ya Lebanon umerejea kwenye mkondo wake wa kawaida.

Mahmoud Az-Zahar ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya habari ya Al-Quds na kubainisha kuwa Hamas inapanua na kustawisha uhusiano wake na Iran na Hizbullah.

Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina amesisitiza kwamba: Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan uko Palestina na ni sehemu ya maeneo ya ardhi hiyo yanayokaliwa kwa mabavu na kwamba karibuni hivi eneo hilo litaainishiwa nafasi yake kulingana na mkakati wa muqawama.

Akizungumzia sababu ya kutoshiriki Hamas kwenye kikao cha kamati kuu ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) kilichofanyika mjini Ramallah, Dakta Az-Zahar amesema: Wao walitaka Hamas ishiriki kikao hicho ili kuitia doa harakati hiyo pamoja na historia yake na kufafanua kwa kusema, harakati ya Fat-h iliyoitisha kikao cha kamati kuu ya PLO inataka HAMAS iridhie kufuata misimamo ya udhalilishaji ambayo inalifuta moja kwa moja suala la Palestina.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniya (kushoto) alipotembelea Iran na kuonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei

Katika sehemu nyengine ya mahojiano hayo na kanali ya satalaiti ya Al-Quds, Az-Zahar amebainisha pia kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ndio uliohusika na shambulio la kigaidi la siku ya Jumapili iliyopita dhidi ya Muhammad Hamdan, mwanachama mwandamizi wa Hamas huko nchini Lebanon.

Hamdan alijeruhiwa baada ya gari iliyotegwa bomu kuripuka katika eneo la Bastan al-Kabir, mjini Saida, kusini mwa Lebanon.../

 

 

Tags