Ismail Haniya: Mapambano dhidi ya Wazayuni yataendelea
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, maamuzi ya Marekani katu hayatabadilisha msimamo wa harakati hiyo.
Ismail Haniya amesisitiza kwamba, maamuzi ya serikali ya Marekani kamwe hayawezi kuwa na taathira yoyote ile kwa msimamo wa harakati ya Hamas.
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza kwamba, hatua za Marekani dhidi ya harakati hiyo si lolote si chochote mbele ya msimamo wa wanamapambano hao wa Palestina na kwamba, mapambano yataendelea kama yalivyo.
Haniya ameongeza kuwa, hatua za Marekakni dhidi ya Hamas ni za bure kwani harakati hiyo haina mpango wa kulegeza kamba wala kuachana na malengo yake matukufu.
Amesema, Hamas katu haitabadilisha misimamo na siasa zake na kwamba, mashinikizo ya Marekani dhidi ya harakati hiyo yanazidi kuifanya ijizatiti zaidi na kuwa imara.
Ismail Haniya kwa mara nyingine tena amesisitiza kwamba, wanapambano wa Hamas hawataruhusu njama za Marekani zinazojulikana kama "Muamala wa Karne" zitekelezwe kivitendo.
Jumatano iliyopita, Wizara ya Hazina ya Marekani iliyaweka majina ya viongozi kadhaa wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) akiwemo kiongozi wa harakati hiyo Ismail Haniya katika orodha ya vikwazo vya Marekani. Akizungumzia hatua hiyo, Haniya alinukuliwa akisema ni fakhari kubwa kwake kuwekwa katika orodha nyeusi ya Marekani.