Amnesty International yakosoa oparesheni za jeshi la Misri huko Sinai
(last modified Thu, 15 Feb 2018 15:55:19 GMT )
Feb 15, 2018 15:55 UTC
  • Amnesty International yakosoa oparesheni za jeshi la Misri huko Sinai

Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limesema kuwa Misri ni lazima iache kutumia mabomu ya vishada haraka iwezekanavyo baada ya jeshi la nchi hiyo kutoa mkanda rasmi wa video unaoonyesha silaha waliozotumia katika oparesheni za hivi karibuni huko Sinai ya Kaskazini.

Taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imesema kuwa, wataalamu wake wameichambua video hiyo na kufikia natija kwamba, mkanda huo umewaonyesha wanajeshi wa Jeshi la Anga la Misri tarehe 9 mwezi huu wakipakia mabomu ya vishada yaliyopigwa marufuku kimataifa katika ndege za nchi hiyo. Jeshi la Misri tarehe 9 mwezi huu wa Februari lilianzisha oparesheni kubwa huko Sinai ya kaskazini kwa kile ilichokitaja kuwa kuyaangamiza makundi ya wanamgambo wenye silaha.

Jeshi la Misri likiwa na magari ya deraya katika oparesheni mkoani Sinai Februari 9 2018 

Mabomu hayo ya vishada aina ya CBU-87 yametajwa kuwa yameundwa nchini Marekani. Mabomu hayo yana madhara makubwa ya muda mrefu na ndio maana yamepigwa marufuku kimataifa.

Hayo yameelezwa na Najia Bounaim, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Amnesty International katika  eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika. Taarifa ya Amnesty pia imeikosoa Marekani kwa kuiuzia Misri mabomu hayo ya vishada yaliyopigwa marufuku. 

Watu walioshuhudia wameeleza kuwa, mwaka 2015 ndege za kivita za Misri aina ya F-16 zilifanya mashambulia ya anga katika maeneo yenye wakazi wengi huko Sinai ambapo makumi ya watoto waliuawa na wengine kujeruhiwa.  

Tags