Wapalestina 148 wajeruhiwa katika makabiliano na wanajeshi wa Kizayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i40503-wapalestina_148_wajeruhiwa_katika_makabiliano_na_wanajeshi_wa_kizayuni
Wapalestina wasiopungua 148 walijeruhiwa Ijumaa wakati wakikabiliana na wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 17, 2018 17:22 UTC
  • Wapalestina 148 wajeruhiwa katika makabiliano na wanajeshi wa Kizayuni

Wapalestina wasiopungua 148 walijeruhiwa Ijumaa wakati wakikabiliana na wanajeshi wa Utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa Hilali Nyekundu ya Palestina, Wapalestina hao wamejeruhiwa katika maandamano ambayo yamekuwa yakifanyika kila Ijumaa kupinga hatua  ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza  Quds (Jerusalem) kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.

Katika maandamano ya jana Wapalestina 125 wamejurhiwa katika makabiliano na Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika miji mbali mbali ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan hasa katika miji ya Ramallah, Al Bireh, Al Khalil na Ariha. Waliosalia wamejeruhiwa katika Ukanda wa Ghaza.

Rais Trump wa Marekani (kushoto) ameutangaza Mji wa Quds uliko Msikiti wa Al Aqsa kuwa eti ni mji mkuu wa utawala bandia wa Israel

Itakumbukwa kuwa, licha ya upinzani mkubwa kieneo na kimataifa, tarehe 6 Desemba mwaka 2017, Rais wa Marekani alitangaza kuwa: Marekani inaitambua rasmi Quds kuwa mji mkuu wa Israel.

Mji wa Quds ni mahali ulipo msikiti mtukufu wa Al Aqsa ambao ni kibla cha mwanzo cha Waislamu na ni sehemu isiyotenganika na ardhi ya Palestina na ni moja ya maeneo matatu makuu matakatifu ya Kiislamu yenye hadhi na umuhimu maalumu mbele ya Waislamu.

Mji huo ulivamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967.