Kuendelea mashambulizi ya Saudi Arabia Yemen; raia watano wauawa mkoani Ta'iz
Raia watano jana usiku waliuawa katika mashambulizi ya ndege za kivita za utawala wa Saudia katika mkoa wa Taiz Yemen.
Ndege za kivita za utawala vamizi wa Saudia jana usiku zililishambulia lori moja na raia watano katika barabara ya al Waziyeh katika kijiji cha Maqbanah mkoani Ta'iz na kusababisha vifo vya raia hao. Mashambulizi dhidi ya raia katika wilaya zinazopatikana katika pwani ya mkoa wa Ta'iz yameongezeka katika siku za hivi karibuni na hadi kufikia sasa makumi ya raia wameuawa na kujeruhiwa.
Kikosi cha makombora cha jeshi la Yemen na makundi ya kujitolea ya wananchi wamejibu mashambulizi ya Saudia kwa kuwauwa na kuwajeruhi mamluki kadhaa wa Saudi Arabia kupitia oparesheni waliyofanya katika mkoa wa Saada kaskazini mwa Yemen. Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi huko Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa kuungwa mkono na Marekani na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, baharini na anga. Ndege za kivita za Saudia hadi sasa zimeuwa na kujeruhi makumi ya maelfu ya raia wa Yemen na kupelekea mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.