UN: Hali ya kimaisha ya Wayemeni ni maafa matupu
Afisa wa operesheni za misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuwa, hali ya kimaisha ya watu wa Yemen ni maafa matupu kutokana na vita vya Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo, njaa na maradhi ya kipindupindu.
John Jing ameliambia Baraza l;a Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba baada ya miaka mitatu ya vita, Yemen imetumbukia katika maafa makubwa na kwamba tangu mwezi Novemba mwaka uliopita watu wengine laki moja wamekimbia makazi yao, suala linalozidisha hali mbaya ya raia wa nchi hiyo.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, Wayemeni milioni 22 na laki mbili wanahitajia misaada ya chakula na kwamba milioni 8 na laki nne miongoni mwao wanakaribia kukumbwa na baa la njaa.
John Jing amesema kuwa, tangu mwezi Aprili mwaka jana raia milioni moja na laki moja wa Yemen wamepatwa na ugonjwa wa kipindupindu.
Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Kiarabu zinazoungwa mkono na Marekani mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen na kuiweka nchi hiyo chini ya mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani. Maelfu ya wananchi wa Yemen wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Miundombinu ya Yemen pia imeharibiwa pakubwa kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.