Hamas: Kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni dhambi isiyosameheka
(last modified Wed, 07 Mar 2018 07:33:07 GMT )
Mar 07, 2018 07:33 UTC
  • Hamas: Kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ni dhambi isiyosameheka

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imesema kwamba, kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ni kinyume na matakwa ya mataifa ya Kiislamu na ni kosa lisilosameheka.

Hayo yamo katika tamko rasmi la harakati ya HAMAS ambayo imeashiria pia namna wananchi wa ulimwengu wa Kiislamu wanavyopinga uhusiano wa aina yoyote ile na utawala wa Kizayuni na kuzilaumu baadhi ya nchi na makundi ya watu wanaoweka uhusiano wa kawaida na Israel kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja.

Harakati ya HAMAS aidha imesema, hatua ya baadhi ya nchi na makundi ya kuongeza kasi ya kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel katika kipindi hiki nyeti sana cha umri wa Palestina ni kujaribu kuhalalisha uwepo wa wavamizi hao wa Palestina katika fikra za vijana wa leo.

Baadhi ya nchi za Kiarabu zimekuwa zikidhihirisha wazi uhusiano wao na utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Itakumbukwa kuwa nchi kama Saudi Arabia zimekuwa zikidhihirisha waziwazi ushirikiano wao na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi nchi nyingine za Kiislamu kama Iran kwa madai kuwa eti nchi hizo zinaingilia masuala ya ndani ya Waarabu.

Harakati ya HAMAS imeushukuru umma wa Kiislamu kwa msimamo wake thabiti kuhusu Palestina na kutaka uungaji mkono huo uendelee kwa ajili ya kulinda haki za wananchi wa Palestina na kupambana na utawala pandikizi wa Israel.

Itakumbukwa pia kuwa, katika miezi ya mwishoni mwa mwaka 2017, baadhi ya nchi za Kiarabu kama Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Saudi Arabia na Bahrain zilivuka mistari yote myekundu katika kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tags