Wayemen 1,300 wameambukizwa Dondakoo huku Saudia ikizidisha hujuma
Shirika la Afya Duniani limetahadharisha kuwa Yemen inashuhudia kwa kasi ugonjwa wa dondakoo (diphtheria) ambao husababisha kupumua kwa shida.
Taarifa ya WHO inasema watu 1,300 wana ugonjwa huo hatari wa kuambukiza ambao sasa umeenea katika maeneo yote ya Yemen, miezi sita baada ya kuripotiwa katika nchi hiyo inayokumbwa na vita.
Hadi sasa watu 70 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo ambapo zaidi ya asilimia 80 ya walioambukizwa ni watoto.
Saudi Arabia ambayo inaungwa mkono kikamilifu na Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa nchi kavu, baharini na angani.
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi tangu Saudia iivamie kijeshi nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Miundombinu ya Yemen pia imeharibiwa pakubwa kufuatia uvamizi wa kijeshi wa Saudi Arabia.