HAMAS yashangazwa na matamshi ya Abbas kwamba ilitaka kumuua Rami Hamdallah
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeshangazwa na matamshi ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Mahmoud Abbas aliyedai kwamba harakati hiyo ilijaribu kumuua Waziri Mkuu wa Serikali ya Ndani ya Palestina, Rami Hamdallah akiwa safarini katika Ukanda wa Ghaza.
Taarifa iliyotolewa na harakati hiyo leo Jumanne imesema kuwa, matamshi ya Abbas yanakinzana na maridhiano ya kitaifa na kwamba lengo la matamshi hayo ni kutaka kuwapigisha magoti wakazi wa ukanda huo. Aidha HAMAS imeonya kwamba, matamshi na misimamo ya rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, yanaweza kuvuruga maridhiano hayo ya kitaifa, kufumbia macho nafasi ya Misri katika maridhiano hayo na pia kuongeza kiwango cha tofauti sambamba na kusambaratisha umoja na mshikamano wa taifa la Palestina.
Katika taarifa hiyo, HAMAS imezitaka pande mbalimbali za eneo hili, za kimataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kuingilia kati mzozo uliozuka kati ya Wapalestina. Hatua hiyo imekuja baada ya Mahmoud Abbas kuituhumu Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kwa kupanga njama kwa ajili ya kumuua Rami Hamdallah na Mkuu wa Idara ya Intelejensia ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina, Majid Faraj wakati walipokuwa safarini katika Ukanda wa Ghaza. Katika tuhuma hizo, Abbas amedai kwamba HAMAS haina nia njema ya kufikiwa maridhiano ya kitaifa kwa ajili ya Palestina, matamshi ambayo yamekadhibishwa vikali na harakati hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo awali harakati hiyo na ofisi ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Ndani ya Palestina ziliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ndio uliopanga shambuliizi lililolenga msafara wa Waziri huyo Mkuu, Rami Hamdallah akiwa safarini katika Ukanda wa Ghaza. Naye kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge la Palestina, Ahmad Bahr alisema kuwa, shambulizi hilo ni uhalifu unaotaka kuharibu mapatano ya Wapalestina, na kutoa mwito wa kufanyika uchunguzi mara moja na kubaini wahusika na kisha kuwachukulia hatua.