Jeshi la Israel lawateka nyara makumi ya Wapalestina
Vikosi vya utawala wa Kizayuni vimewateka nyara makumi ya Wapalestina wakiwemo wanawake, katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan linalokaliwa kwa mabavu.
Katika operesheni ya usiku kucha, wanajeshi wa utawala haramu wa Israel wameshambulia nyumba za Wapalestina katika baadhi ya miji huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi na kuwatia mbaroni Wapalestina zaidi ya 40.
Duru za habari zinasema, uvamizi huo wa jeshi katili la Israel umefanyika katika miji ya Jenin, Qalqilya na Quds Tukufu, ambapo Wapalestina 43 wametiwa nguvuni, wengi wakiwa ni wake na waume zao.
Mapema mwezi huu wa Machi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake, Ripoti ya Kamisheni ya Wafungwa wa Kipalestina ilibanisha kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umewatia mbaroni wanawake wasiopungua 15,000 wa Kipalestina tokea mwaka 1967 hadi sasa.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za wafungwa la Addameer, Wapalestina 6,500 wanazuiliwa katika jela za Israel tangu Januari mwaka huu hadi sasa, wakiwemo watoto wadogo na wanawake zaidi ya 350.
Wafungwa hao wa Kipalestina wamekuwa wakilalamika kuwa wanateswa na kudhalilishwa katika magereza hayo ya kuogofya ya utawala katili wa Israel.