Gholamali Khoshroo aitaka Saudi Arabia iachane na vita
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameutaka utawala wa Aal Saud wa Saudi Arabia uachane na hatua zake za vita.
Gholamali Khoshroo amesema hayo akijibu hatua ya kichekesho ya jana ya Saudi Arabia ya kuutumia barua Umoja wa Mataifa ikieleza kwamba, makombora yaliyorushwa kuelekea Riyadh kutokea Yemen yametengenezwa nchini Iran na kueleza kwamba, hii si mara ya kwanza kwa Saudia kuandika barua kama hizo lengo likiwa ni kufunika kushindwa kwake huko Yemen.
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa sambamba na kusisitiza kwamba, hatua ya Saudi Arabia ya kuishambulia kijeshi nchi ya Yemen imesababisha njaa na maafa ya kibinadamu kwa wananchi wa nchi hiyo ameeleza kuwa, watawala wa Saudi Arabia wakiwa na lengo la kufunika jinai zao nchini Yemen daima wamekuwa wakiituhumu Iran kwa tuhuma ambazo hazina msingi wowote.
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, daima Iran imekuwa ikisisitiza kwamba, hakuna njia nyingine yoyote ile ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Yemen isipokuwa utatuzi wa kisiasa.
Saudi Arabia na washirika wake waliivamia Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa kisingizio cha kumrejesha madarakani kibaraka wa Riyadh, Abdrabbuh Mansur Hadi aliyetoroka nchi na kukimbilia Riyadh. Kufuatia hujuma hiyo, maelfu ya raia wa Yemen wameuawa hadi sasa na mamilioni ya wengine wamelazimika kuwa wakimbizi.