Mabomu elfu moja ya kutegwa ardhini yapatikana Kirkuk, Iraq
Kundi la kujitolea la wananchi wa Iraq la al Hashdu al Sha'abi limearifu kuwa limepata mabomu elfu moja ya kutegwa ardhini yaliyoundwa nchini Ujerumani kupitia operesheni ya usalama kusini magharibi mwa mkoa wa Kirkuk huko Iraq.
Kundi la Hashdu al Sha'abi limetangaza kuwa, kikosi chao cha 15 kimegundua eneo moja lenye maficho ya silaha na zana za kivita; ambako ndani yake wamekuta pia mabomu elfu moja ya kutegwa ardhi yaliyoundwa nchini Ujerumani yanayoitwa Falmara pamoja na zana nyingine za kijeshi.
Oktoba 16 mwaka jana jeshi la Iraq liliudhibiti mji wa Kikruk ambao awali ulikuwa mikononi mwa wapiganaji wa Kikurdi wa Pishmerga. Habari nyingine zinaeleza kuwa, afisa mmoja wa Iraq amesema kuwa baada ya kuwasiliana Baghdad na Ankara na kufuatia malalamiko ya Uturuki kwamba, wapiganaji wa Kikurdi wa PKK wako katika mji wa Sinjar, vikosi vya jeshi la Iraq hivi sasa viko katika kivuko cha mpakani cha Khansur baada ya Baghdad kukidhibiti kivuko hicho kutoka kwa kundi la waasi wa PKK wa Uturuki.
Jana pia maafisa wa Iraq mjini Baghdad walitangaza kufikia mapatano ya awali kati ya serikali ya Iraq na wa upande wa Uturuki kuhusu hali ya mambo katika mji wa Sinjar ulioko umbali wa takriban kilomita 80 magharibi mwa mji wa Mosul na kuwepo katika mji huo wapiganaji wa Kikurdi wa PKK.