Saudia inapanga kuigeuza Qatar kisiwa na jalala la takataka za nyuklia
Saudi Arabia inapanga kuanzisha mradi wa ujenzi wa mfereji kwenye mpaka wake wa pamoja wa ardhini na Qatar ambao utaigeuza nchi hiyo ndogo ya Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi kuwa kisiwa.
Magazeti ya Sabq na Al-Riyadh yanayochapishwa nchini Saudia yameripoti katika matoleo yao ya jana kuwa utawala wa Aal Saud umekusudia kujenga mfereji unaofanana na ule wa Suez wa Misri katika mpaka wake wa ardhini na Qatar ili kuifungia kikamilifu mpaka wa ardhi nchi hiyo na kuigeuza kisiwa.
Eneo la mfereji huo linakusudiwa kutumiwa kama sehemu za burudani na starehe kwa watalii, michezo ya majini na pia kwa ajili ya miradi ya kiuchumi na sekta ya mafuta ili kuibana na kuipa changamoto kali zaidi Qatar.
Mbali na mfereji huo utakaounganishwa na eneo la bahari kuigeuza nchi ya peninsula ya Qatar kuwa kisiwa, utaugeuza pia mpaka wake mmoja tu wa ardhini kuwa eneo la kijeshi la Saudia na jalala la kutupia takataka za nyuklia za vinu vya nyuklia ambavyo nchi hiyo ina mpango wa kujenga. Imeelezwa kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati (UAE) nao pia unapanga kujenga jaa la takataka za nyuklia karibu kabisa na mpaka wake wa pamoja na Qatar.
Kwa mujibu wa gazeti la Sabq, kama utatekelezwa, ujenzi wa mfereji huo unaotazamiwa kupewa jina la Mfereji wa Baharini wa Salwa utakamilika katika muda wa mwaka mmoja tu.
Aidha wawezekaji kutoka Saudi Arabia na Imarati ndio wanaotazamiwa kuufadhili kifedha, na uchimbaji wake utafanywa na makampuni ya Misri yenye uzoefu wa shughuli za ujenzi wa Mfereji wa Suez wa nchi hiyo.
Mradi huo unaotafsiriwa kama hatua ya kiuadui dhidi ya Qatar utagharimu karibu dola milioni 750 za Marekani na mfereji wenyewe utakuwa na urefu wa kilomita 60, upana wa mita 200 na kina cha mita 20.
Waziri wa Nchi wa Imarati anayehusika na mambo ya nje Anwar Gargash amedai kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa mradi huo ni "ithbati kwamba Qatar imeshindwa kuushughulikia na kuutatua mgogoro wake" na kwamba kimya kilichoonyeshwa na serikali ya Doha hadi sasa juu ya suala hilo ni "ushahidi wa hofu na mkanganyo ulioipata" serikali hiyo.
Ikumbukwe kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudi Arabia, Imarati, Bahrain na Misri zilichukua hatua ya kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Qatar na kuiwekea vikwazo vya nchi kavu, baharini na angani nchi hiyo kwa tuhuma kwamba serikali ya Doha inaunga mkono ugaidi.../