Apr 12, 2018 02:34 UTC
  • Kushadidi siasa za kibaguzi za Aal Saud nchini Saudi Arabia

Kwa akali watu watatu wametiwa mbaroni kufuatia hujuma ya askari wa utawala wa Aal Saud katika mji wa Qatif ulioko katika mkoa wa ash-Sharqiyah nchini Saudi Arabia.

Mji wa Qatif kutokana na wakazi wake kuwa ni Waislamu wa madhehebu ya Shia daima umekuwa ukikabiliwa na dhulma na ubaguzi. Hii ni katika hali ambayo, mji huo kutokana na kuwa na vyanzo vya utajiri kama nishati ya mafuta na kudhamini sehemu muhimu ya pato la utawala wa Aal Saud umekuwa na nafasi maalumu kwa nchi hiyo.

Siku zote mji wa Qatif umekuwa ukilengwa na hujuma na mashambuluio ya askari wa utawala wa Aal Saud ambapo hadi sasa makumi ya wakazi wa mji huo wameuawa na mamia ya wanaharakati wa masuala ya kiraia na kisiasa wametiwa mbaroni. Takribani Mashia nchini Saudi Arabia wanaunda asilimia 10 hadi 15 ya wakaazi wa nchi hiyo ya Kiarabu ambapo kwa kawaida Waislamu hao wa Kishia wanapatikana katika mkoa wa ash-Sharqiyah. 

Muhammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia

Tangu mwaka 2011 eneo la mashariki mwa Saudi Arabia  limekuwa likishuhudia wimbi la malalamiko  dhidi ya utawala wa Aal Saud ya kupinga dhulma na kutaka kuweko ugawaji sawa na wa kiadilifu wa utajiri wa nchi hiyo. Miamala iliyo dhidi ya ubinadamu ya watawala wa Aal Saud dhidi ya wapinzani na jamii ya waliowachache katika nchi hiyo inabainisha kilele cha ubaguzi wa watawala wa nchi hiyo.

Matukio ya kisiasa nchini Saudi Arabia yanaonyesha kuwa, kubadilishwa viongozi hakupelekei kutokea mabadiliko ya kimsingi katika  siasa za utawala huo wa kibedui ambao umejengeka juu ya misingi ya udikteta.

Kushadidi ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia na kutokuweko matumaini yoyote ya watawala hao kubadilisha siasa zao, kumeongeza wasiwasi wa kukanyagwa zaidi haki za binadamu katika nchi hiyo. Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, kile kinachofanyika nchini Saudia na kuonekana kama ni marekebisho makubwa, si kingine ghairi ya hatua zinazofanyika kwa lengo la kuficha ukiukaji wa haki za binadamu wa Riyadh na hakuna mtu atakayehadaika na hilo.

Shirika la Msamaha Duniani,  Amnesty International

Shirika hilo la Amnesty International limesisitiza kwamba: Hatua ya Saudi Aarabia ya kubadilisha sura na nafasi ya nchi hiyo ambayo ina doa jeusi la kufanya ukandamizaji wa uhuru wa kutoa maoni na kuishambulia kijeshi Yemen, haiwezi kumhadaa mtu yeyote.

Samah Hadid, Mkurugenzi wa Amnesty International kitengo cha Mashariki ya Kati ametangaza kuwa: Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ametekeleza majukumu kama mrekebishaji lakini ukandamizaji dhidi ya wapinzani umeongeza mno tangu alipochukua wadhifa huo. Ali al-Ahmad mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuwa, kuna haja kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kukabiliana na siasa za Saudia na kubainisha kwamba, utawala wa Riyadh ni mithili ya ulivyokuwa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini wa Apartheid.

Mweledi huyo wa masuala ya kisiasa ambaye ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Ghuba ya Uajemi amesema akiwa Washington Marekani kwamba, kama ambavyo katika utawala wa Apartheid, wazalendo weusi wa Afrika Kusini hawakuwa na haki ya kutangaza uwepo wao, nchini Saudi Arabia pia, Waislamu wa Kishia wanabinywa na hawawezi kuonyesha kwa uhuru uwepo wao.

Mashambulio ya jeshi la Saudi Arabia katika mji wa Qatif

Hata kama ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud unajumuisha raia wote wa Saudi Arabia, lakini Mashia wa nchi hiyo wamekuwa wakikandamizwa zaidi wakilinganishwa na raia wengine wa nchi hiyo ya Kiarabu. Mtazamo wa kibaguzi wa Aal Saud ndio ambao umewafanya watawala wa Riyadh wawatizame Mashia wa nchi hiyo kama raia wa daraja la pili.

Mtazamo huo umewafanya Waislamu hao wa Kishia kunyimwa haki za kimsingi na za awali kabisa za kiraia na hivyo kukabiliwa na ubaguzi wa kila upande.

Wakati Mashia wa Saudia wananyimwa hata uhuru wa kutoa maoni, watawala wa nchi hiyo wamekuwa wakitumia fedha zinazotokana na kipato cha mafuta na katika sekta nyingine kwa ajili ya kueneza fikra potofu za Kiwahabi.

Mfalme Salman bin Abdul-Aziz wa Saudi Arabia

Takwimu zinaonyesha kuwa, watawala wa Aal Saud wamekuwa wakitumia fedha nyingi mno kwa ajili ya kueneza fikra za Kiwahabi ambazo chimbuko lake ni itikadi za ugaidi, utakfiri na utumiaji mabavu.

Licha ya utendaji huo mbaya wa kibaguzi wa Saudi Arabia pamoja na jinai zake huko Yemen, hivi karibuni nchi hiyo ikipata uungaji wa madola ya Magharibi kama Marekani na Uingereza, kwa mara nyingine tena ilipata uanachama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Utendaji huu wa kindumakuwili wa Umoja wa Mataifa haujawa na natija nyingine bighairi ya kuwapa kichwa na kiburi watawala wa Riyadh cha kukiuka zaidi haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Tags