Saudia: Sharti serikali ya Qatar itume vikosi Syria ili isipinduliwe
(last modified Wed, 25 Apr 2018 07:27:20 GMT )
Apr 25, 2018 07:27 UTC
  • Saudia: Sharti serikali ya Qatar itume vikosi Syria ili isipinduliwe

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amesema iwapo serikali ya Qatar inataka isiondolewe madarakani na iendelee kudhaminiwa usalama na Marekani, sharti itume wanajeshi wake nchini Syria.

Adel Jubeir amesema serikali ya Doha haiwezi kubakia hai hata wiki moja iwapo Marekani itaamua kusimamisha uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Qatar.

Amesema, "Doha lazima itume vikosi vyake Syria kabla Rais wa Marekani hajafuta Kinga ya Marekani kwa Qatar, inayojumuisha uwepo wa kituo cha kijeshi cha Marekani katika nchi hiyo ya Kiarabu."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia amebainisha kuwa, iwapo Marekani itaamua kuondoa wanajeshi wake wapatao elfu 10 katika kituo cha jeshi la anga cha Al-Udeid karibu na mji mkuu Doha, basi serikali ya Qatar itapinduliwa katika muda wa chini ya wiki moja.

Wanajeshi wa Qatar

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia na washirika wake yaani Misri, Imarati na Bahrain ilitangaza kuiwekea vikwazo Qatar hapo tarehe tano Juni mwaka jana baada ya serikali ya Doha kupinga kuburuzwa na Riyadh.

Mbali na kuiwekea vikwazo Qatar, nchi hizo ziliiwekea pia mzingiro wa baharini, angani na nchi kavu. Tarehe 23 mwezi huo huo mwaka jana, nchi hizo zilitangaza masharti 13 zikiitaka Qatar kuyatekeleza ili kufunguliwa upya uhusiano ya pande mbili, suala ambalo limepuuzwa na Doha.

Tags