Nabih Berri atahadharisha kuhusu Israel kuishambulia Lebanon
Spika wa Bunge la Lebanon ametahadharisha kwamba, utawala haramu wa Israel umeajiandaa kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu.
Nabih Berri amesema hayo kusini mwa Lebanon na kueleza kwamba, Israel imeandaa na kuziweka tayari na kwa siri suhula zake za kivita kwa ajili ya kufanya uvamizi wa kijeshi nchini Lebanon.
Spika wa Bunge la Lebanon ameongeza kuwa, Wazayuni wanapanga kuishambulia kijeshi Lebanon ili kuirejesha nyuma nchi hiyo.
Rais Michel Aoun wa Lebanon nae ameonya mara kadhaa juu ya matokeo mabaya endapo utawala haramu wa Israel utathubutu kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Kiarabu.
Hayo yanajiri katika hali ambayo kumekuwa kukiripotiwa mara kwa mara habari za kuweko uwezekano wa Israel kuishambulia kijeshi Lebanon katika mwaka huu.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Mkuu wa Jeshi la Utawala Haramu za Israel, Gadi Eizenkot alinuukuliwa akisema kuwa, kuna uwezekano mkubwa utawala huo ukapigana vita vikali na angamizi kati yake na Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya nchini Lebanon.
Habari za uwezekano wa kuingia vitani Israel na Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon zinaripotiwa katika hali ambayo, katika vita vya siku 33 vilivyoanza mwezi Julai 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni lilipata pigo kubwa kutoka kwa wanamuqawama wa Hizbullah.
Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah amekuwa akisisitiza kuwa, endapo Israel itaanzisha vita vyovyote dhidi ya Lebanon, basi muqawama utahakikisha vita hivyo vinapiganwa ndani ya utawala haramu wa Kizayuni.