HAMAS yasisitiza kuendeleza uhusiano wa kistratejia na nchi zinazouhami Muqawama
(last modified Sat, 05 May 2018 14:56:40 GMT )
May 05, 2018 14:56 UTC
  • HAMAS yasisitiza kuendeleza uhusiano wa kistratejia na nchi zinazouhami Muqawama

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitizia ulazima wa kuendelezwa uhusiano wa kistratejia na nchi zinazounga mkono na kuuhami muqawama wa Palestina.

Mahmoud Az-Zahar, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Hamas ameiambia kanali ya televisheni ya Al-Alam kuwa kuna ulazima wa kuendeleza uhusiano wa kistratejia na nchi zinazoihami na kuiunga mkono Palestina zikiongozwa na Iran ili kufikia hatua itakayowezesha kuthibiti malengo makuu ya muqawama ambayo ni kuikomboa Palestina.

Dakta Az-Zahar amesisitiza kuwa Wapalestina wataikomboa ardhi yao yote na hiyo ndiyo sha'ar na wito wa shime wa muqawama. Amesema lengo hilo haliwezi kufikiwa kwa kufanya ujasusi au kushirikiana kiusalama na Israel na kwamba njia pekee itakayowezesha kukombolewa Palestina ni kutekelezwa mpango wa muqawama ambao unaendeshwa na harakati ya Hamas.

Maandamano ya Haki ya Kurejea yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza

Kiongozi huyo mwandamizi wa Hamas amesisitiza pia kwamba maandamano ya kudai haki ya Wapalestina kurejea kwenye ardhi yao ambayo yangali yanaendelea yamekuwa na mafanikio mengi, ya kwanza ni kwamba, kwa kutekeleza njama iliyopangwa na utawala wa Kizayuni, kuna watu ambao walitaka wananchi wa Palestina waingie barabarani kuandamana dhidi ya muqawama, lakini njama hiyo haikufaulu, na badala yake wananchi hao wameandamana dhidi ya Israel.

Maandamano ya amani ya "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi kwa mnasaba wa "Siku ya Ardhi" huko katika Ukanda wa Gaza na yangali yanaendelea. Hadi sasa Wapalestina 50 wameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Israel na wengine wapatao elfu nane wamejeruhiwa.../   

Tags