Msalaba Mwekundu: Takribani nusu ya hospitali za Yemen zimebomolewa
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu (ICRC) limetangaza kuwa, katika kipindi cha miaka miwili iliyopita zaidi ya mashambulio 1,200 yametekelezwa dhidi ya hospitali, vifaa vya tiba na timu za watoaji huduma za matibabu katika maeneo mbalimbali duniani hususan nchini Yemen.
Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya mashambulio 1,200 yamelenga hospitali, magari ya wagonjwa na wafanyakazi wa huduma za tiba katika nchi 16 duniani.
Taarifa ya shirika hilo imeeleza, hospitali za Yemen ndizo zilizoandamwa zaidi na hujuma za kijeshi ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, karibu nusu ya hospitali za Yemen zimebomolewa kufuatia mashambulio ya anga ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.
Aidha ripoti hiyo inaonyesha kuwa, Syria ni nchi nyingine ambayo hospitali zake nyingi zimebomolewa kufuatia mashambulio ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu.
Saudi Arabia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kumrejesha madarakani Abdrabbuh Mansour Hadi, Rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kutoroka nchi.
Hata hivyo utawala wa Aal Saud na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo, licha ya kusababisha maafa makubwa kwa raia wasio na hatia yoyote na kuharibu miundombinu ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.