Bahrain yawapokonya uraia wapinzani 115, yawafunga jela maisha 53 miongoni mwao
Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa ukandamizaji na mbinyo dhidi ya wapinzani na wakosoaji wa serikali, utawala wa Aal-Khalifa umewavua uraia wananchi 115 wa Bahrain, huku ukiwahukumu kifungo cha maisha jela 53 miongoni mwao.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumanne, mwendesha mashtaka wa umma nchini humo amedai kuwa, watuhumiwa hao wamepatikana na hatia katika mashitaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwaandama.
Aidha amedai kuwa washukiwa hao wamekuwa wakifanya uasi na kuendeleza harakati za kigaidi nchini humo eti kwa uungaji mkono wa Iran.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Wabahrain waliandamana katika pembe tofauti za nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi kulalamikia ukandamizaji wa utawala huo dhidi yao, baada ya utawala huo kutoa hukumu ya kifo dhidi ya vijana sita wa nchi hiyo, ambapo wanne miongoni mwao walikuwa watu wa karibu na watetezi wa Sheikh Isa Qassim, Kiongozi wa Waislamu wa Shia nchini humo.
Katika ripoti yake ya mwaka huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kwamba utawala wa Bahrain ni moja ya tawala kandamizi zaidi duniani na kwamba hali ya haki za binadamu nchini humo mwaka uliopita ilikuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na ya miaka iliyopita.
Bahrain imekuwa ikishuhudia malalamiko ya wananchi tangu tarehe 14 Februari mwaka 2011, ambapo wananchi wanataka kufanyika mabadiliko ya msingi, ingawa utawala wa nchi hiyo umeendelea kupuuza kilio hicho cha wananchi na badala yake kutumia mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa kuyazima.