Amnesty: Ni upuuzi kuwavua uraia Wabahrain 115 katika 'kesi ya umati'
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limekosoa vikali hatua ya hivi karibuni ya Bahrain ya kuwafunga jela na kuwapokonya uraia makumi ya wanaharakati wa kisiasa ambao wanaonekana kuwa wakosoaji wakubwa wa utawala wa Aal-Khalifa.
Lynn Maalouf, Mkurugenzi wa Utafiti eneo la Mashariki ya Kati wa shirika hilo lenye makao yake mjini London nchini Uingereza amesema kuwa, ni upuuzi na jambo lisiloingia akilini kutoa hukumu moja kwa mkusanyiko wa watu, na kuwanyima haki ya msingi ya kusikilizwa kesi zao katika mchakato wa kiuadilifu.
Jumanne iliyopita, Hamad Shaheen, Kaimu Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Jinai za Kigaidi nchini Bahrain, alisema utawala wa Aal-Khalifa umewavua uraia wananchi 115, huku ukiwahukumu kifungo cha maisha jela 53 miongoni mwao, eti kwa kupatikana na hatia katika mashitaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwaandama.
Afisa huyo wa Amnesty International ameongeza kuwa, "Hii ni moja ya hukumu mbaya zaidi kuwahi kutolewa na watawala wa Bahrain, ambao kimsingi hawajali hata chembe viwango vya kimataifa vinavyopaswa kufuatwa katika mchakato wa kesi. Utawala wa Manama unatumia mbinu hiyo ya kuvua uraia kwa lengo la kukandamiza wapinzani na wakosoaji wake."
Bahrain imekuwa ikishuhudia malalamiko ya wananchi tangu tarehe 14 Februari mwaka 2011, ambapo wananchi wanataka kufanyika mabadiliko ya msingi, ingawa utawala wa nchi hiyo umeendelea kupuuza kilio hicho cha wananchi na badala yake kutumia mkono wa chuma na ukandamizaji mkubwa kuyazima.