Wapalestina waitaka ICC ichunguze ukiukaji wa haki za binadamu wa Israel
Palestina imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ianzishe uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel hususan harakati za utawala huo za kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina unaozikalia kwa mabavu.
Faili la malalamiko hayo ya Wapalestina limewasilishwa leo Jumanne katika mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi na Riyadh al-Maliki, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Palestina.
Katika faili hilo lililowasilishwa mbele ya ICC, Wapalestina wameitaka mahakama hiyo ya kimataifa ichunguze harakati za nyuma, za sasa na zinazotarajiwa za Israel za kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ikiwemo mashariki mwa mji mtukufu wa Quds.
Takriban Waisreli laki 6 wanaishi katika vitongoji 230 ambavyo vilijengwa kinyume cha sheria za kimataifa na Wazayuni maghasibu, katika ardhi za Palestina.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa liliafiki kuundwa tume huru ya kuchunguza matukio ya hivi karibuni katika eneo la Gaza na kadhalika matukio ya ukiukaji mkubwa wa haki za Wapalestina uliofanywa na utawala huo katili.
Itakumbukwa kuwa, Jumatatu ya wiki iliyopita, sambamba na kufunguliwa ubalozi wa Marekani mjini Quds (Jerusalem), ambayo pia ni siku iliyoendana na kumbukumbu ya tukio chungu la kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuondolewa kwa nguvu raia hao katika maeneo yao asilia, wakazi wa Ukanda wa Gaza walifanya maandamano makubwa ya amani, ambapo katika maandamano hayo zaidi ya Wapalestina 60 waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa Kizayuni, mbali na wengine zaidi ya elfu mbili kujeruhiwa.