Utawala wa Kizayuni wa Israel wahujumu Ukanda wa Ghaza
Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni wa Israel leo zimetekeleza mashambulizi dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Taarifa zinasema ndege hizo za Wazayuni zimeshambulia kituo cha kijeshi cha Brigedi ya Al Quds, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Jihad Islami.
Hujuma hiyo imetekelezwa baada ya Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kusema kuwa, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, na Jihad Islami ndio wahusika wa hujuma ya maroketi ambayo yamewalenga Wazayuni huko Israel. Aidha amesema utawala huo utatoa jibu kali kufuatia oparesheni hiyo ya makundi ya wapigania ukombozi wa Palestina. Katika upande mwingine, wajumbe wa bunge la utawala haramu wa Israel, Knesset, wametaka mashambulizi makali zaidi yatekelezwe dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
Mapema Jumanne asubuhi, wapigania ukombozi wa Palestina walivurumisha maroketi 22 kuelekea Israel baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuhujumu kwa makombora vituo vya harakati za kupigania ukombozi Palestina. Katika uvamizi huo wa Israel huko Ghaza, Mpalestina mmoja ameuawa shahidi. Tokea Machi 30 hadi sasa, utawala haramu wa Israel umewaua Wapalestina zaidi ya 120 waliokuwa wakishiriki katika maandamano ya kutetea haki ya kurejea katika ardhi zao za jadi.
Hayo yanajiri wakati ambao leo boti kadhaa za Wapalestina katika pwani ya Ukanda wa Ghaza zimefunga safari zenye lengo la kuvunja mzingiro wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya eneo hilo.