Nasrullah asisitiza ulazima wa Waislamu kukabiliana na fitna ya Wasaudi; na Ulimwengu wa Kiislamu kufanya hima ya kuwasaidia watu wa Quds
(last modified Sat, 09 Jun 2018 03:33:44 GMT )
Jun 09, 2018 03:33 UTC
  • Nasrullah asisitiza ulazima wa Waislamu kukabiliana na fitna ya Wasaudi; na Ulimwengu wa Kiislamu kufanya hima ya kuwasaidia watu wa Quds

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema: Njama hatari zaidi ya adui ni mpango wa Marekani wa "Mapatano ya Karne" ambayo lengo lake ni kulitolea hukumu suala la Palestina na kuisalimisha Quds na matukufu yake kwa utawala ghasibu wa Kizayuni.

Sayyid Hassan Nasrullah aliyasema hayo jana alipohutubia maelfu ya watu kusini mwa Lebanon kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Katika hotuba hiyo aliyotoa kwa njia ya vidio katika kijiji cha Marunu-Ra'as kilichoko umbali wa kilomita mbili kutoka kwenye mpaka wa pamoja wa Lebanon na Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel), Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema: Wananchi wa Palestina, makundi ya muqawama na Mamlaka ya Ndani ya Palestina wanakabiliwa na mashinikizo ya kuwataka wayakubali Mapatano ya Karne, hata hivyo baada ya kupita miaka 70 Muqawama wa taifa la Palestina ungali endelevu na wenye damu changa.

Sayyid Hassan Nasrullah ameongeza kuwa: Leo hii Quds inakabiliwa na changamoto tatu; ya kwanza ni ya nchi za ulimwengu kuutambua rasmi utawala wa Kizayuni na kusalimu amri mbele ya uamuzi wa Marekani. Changamoto ya pili inahusu demografia na muundo wa idadi ya watu huko Quds na kubadilishwa utambulisho wa wakaazi wa mji huo mtakatifu; na changamoto ya tatu ni ya suala la matakatifu ya mji wa Quds hususan msikiti wa Al Aqsa na heshima ya msikiti huo uliobarikiwa.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds maeneo mbalimbali duniani

Katibu Mkuu wa Hizbullah ametanabahisha kuwa katika Ulimwengu wa Kiarabu yamejiri matukio ambayo hayajawahi kushuhudiwa katika miaka 70 iliyopita na kufafanua kwa kusema, kuna baadhi ya watu waliotangaza kwa kalamu na ndimi zao kwamba Wazayuni wana haki Palestina na Baitul Muqaddas na kwamba Saudi Arabia ndiyo inayobeba dhima ya msimamo huo. Ameongeza kuwa leo katika eneo la Mashariki ya Kati kuna watu wanataka kulinda tawala zao, na kinachofanywa na watu hao wanaoungwa mkono na Marekani ni kuelekea kwenye mkondo wa kuitambua rasmi Israel.

Sayyid Hassan Nasrullah aidha amebainisha kwamba ni wajibu wa watu wote kuwasaidia kifedha raia wa Palestina katika mji wa Baitul Muqaddas. Ameongeza kuwa Wapalestina wa Quds wana azma thabiti na utayari wa kuendelea kubaki katika mji huo lakini Waislamu nao wanapaswa kutoa msaada kwa wenzao hao.../