Ansarullah: Al-Hudaydah itakuwa makaburi ya askari vamizi
Kiongozi wa ngazi ya juu wa Harakati ya wananchi ya Ansarullah nchini Yemen amesema kuwa, shambulizi dhidi ya meli ya kivita ya Saudi Arabia katika pwani ya al-Hudaydah ni jibu imara dhidi ya wavamizi linalotoa ujumbe wa wazi kwamba, eneo hilo litakuwa makaburi ya askari vamizi.
Dhaifullah al-Shami, mjumbe wa Idara ya Siasa ya harakati hiyo ya Yemen aliyasema hayo Alkhamisi ya jana katika mahojiano na Shirika la Habari la Mehr na kusisitiza kwamba, Yemen ni taifa la muqawama ambalo kamwe halikubali kusalimu amri, bali limejiandaa kukabiliana vilivyo na uvamizi wa Marekani, Israel, Saudia na Imarati.
Al-Shami amesema kwamba Wayemeni wanaamini kwamba vita hii lazima imalizike kwa maslahi ya taifa lao na kwamba maadui yaani Marekani, Wazayuni na Aal-Saud hawawezi kupata ushindi. Ameongeza kwamba Wasaudi, Imarati na Wamarekani wanapata pigo katika nyanja tofauti kutoka kwa raia shupavu wa Yemen kiasi kwamba sasa Wamarekani wamelazimika kuingia vitani moja kwa moja kwa kusimamia mashambulizi ya Saudia. Mjumbe wa Idara ya Siasa ya Ansarullah ameashiria kimya cha Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuhusiana na jinai zinazotendwa na wavamizi nchini Yemen na kusema, ni suala la kusikitisha kwamba, UN na Baraza lake la Usalama zipo katika njia moja na Marekani kuhusiana na suala hilo.
Mwezi uliopita askari wa Saudia na Imarati walianzisha mashambulizi makali yenye lengo la kuidhibiti bandari muhimu ya al-Hudaydah. Hata hivyo jeshi la Yemen kwa kushirikiana na Harakati ya Wananchi ya Ansarullah wametoa pigo kali dhidi ya askari hao vamizi katika siku za hivi karibuni sambamba na kusambaratisha pia meli ya kivita ya Saudia katika eneo hilo.