Syria: Magaidi wanashirikiana na Wazayuni kubomoa nyumba za Wapalestina wanaoishi Syria
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Faisal Miqdad amesema kuwa wanachama wa makundi ya kigaidi na ukufurishaji kwa uungaji mkono wa utawala haramu wa Kizayuni, wanabomoa nyumba za Wapalestina walioko Syria.
Miqdad aliyasema hayo Jumatatu ya jana mjini Damascus, mji mkuu wa Syria alipokutana na Pierre Krähenbühl, Mkurugenzi wa Shirika la Misaada na Kubuni kazi kwa ajili ya Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) na kuongeza kuwa, katika mgogoro unaoendelea nchini humo kwa mara kadhaa makundi ya kigaidi yameshambulia kambi za wakimbizi wa Kipalestina sambamba na kuharibu nyumba na ofisi zao. Aidha Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria amesema kuwa, magaidi hao wanaopata uungaji mkono kamili kutoka Israel wamewaua Wapalestina wengi wanaoishi nchini Syria.
Ameongeza kwamba serikali ya Syria inalipa umuhimu wa kipekee suala la Wapalestina na kwa ajili hiyo inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuondokana na mzozo huo sambamba na kuwapunguzia machungu wakimbizi wa Palestina walioko nchini humo. Amezidi kufafanua kuwa, utawala haramu wa Kizayuni ni muhusika mkuu wa tabu na mashaka wanayoyapata raia wa Palestina na pia kuwanyima haki zao za msingi na amelaani vikali kitendo cha Marekani kusimamisha misaada yake na kuacha kutekeleza ahadi zake kuhusiana na bajeti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada kwa ajili ya Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). Amesema kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa lengo la kudhamini maslahi ya utawala katili wa Kizayuni na kuifanya hali ya Wapalestina kuwa mbaya zaidi.