Utayarifu wa Yemen kwa ajili ya kushadidisha mashambulizi dhidi ya wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46620-utayarifu_wa_yemen_kwa_ajili_ya_kushadidisha_mashambulizi_dhidi_ya_wavamizi
Mohammed Abdulsalam msemaji rasmi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amebainisha kwamba vikosi vya kujitolea vya wananchi na jeshi la nchi hiyo vipo tayari kushadidisha mashambulizi dhidi ya muungano vamizi unaoongozwa na Marekani na Saudi Arabia katika maeneo mbalimbali ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 07, 2018 11:01 UTC
  •  Utayarifu wa Yemen kwa ajili ya kushadidisha mashambulizi dhidi ya wavamizi

Mohammed Abdulsalam msemaji rasmi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amebainisha kwamba vikosi vya kujitolea vya wananchi na jeshi la nchi hiyo vipo tayari kushadidisha mashambulizi dhidi ya muungano vamizi unaoongozwa na Marekani na Saudi Arabia katika maeneo mbalimbali ya Yemen.

Saudi Arabia huku ikiungwa mkono na Imarati, Marekani, utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi nyingine waitifaki wake tangu mwezi Machi mwaka 2015 ilianzisha hujuma ya kijeshi huko Yemen na kisha kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa ardhini, majini na baharini. Utawala wa Saudi Arabia na nchi waitifaki wake hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yao ya kumrejesha madarakani kibaraka wao huko Yemen kutokana na muqawama ulioonyeshwa na wananchi dhidi ya nchi hizo vamizi. Mashambulizi makubwa ya kijeshi yanayotekelezwa na muungano vamizi wa Saudia huko Yemen hatimaye yamewapelekea wanamuqawama wa Ansarullah kujibu chokochoko hizo za wavamizi kwa kuvurumisha makombora dhidi ya muungano huo; stratejia ya kijeshi ambayo imewashtua na kuwatia hofu kubwa watawala wa Saudia. Kuvurumishwa makombora hayo ya balistiki ya Yemen ni nukta muhimu katika mapambano ya wanamuqawama wa Yemen dhidi ya uvamizi wa Saudia; na imedhihirisha uwezo wa ndani wa Wayemeni wa kuzulisha makombora mkabala na wavamizi. 

Maeneo ya kurushia makombora ya chini ya ardhi ya jeshi la Yemen 

Kuhusiana na suala hilo, tovuti ya al Ahad ya Lebanon imemnukuu Ismail Al Muhaqari akisema kuwa muungano vamizi wa Saudia unaendelea kukabiliwa na kibarua kigumu. Kushindwa katika pwani ya magharibi, kuongezeka kiwango cha oparesheni za ndege zisizo na rubani, mashambulio mtawalia ya makombora ya balistiki na hatimaye kuzinduliwa maeneo ya kurushia makombora ya chini ya ardhi ni miongoni mwa kibarua hicho kigumu. Kutangazwa kuwepo maeneo hayo ya chini ya ardhi wakati huu ni mafanikio maalumu yanayoimarisha stratejia ya kiulinzi ya nguvu ya makombora ya Yemen sambamba na kupanua machaguo na oparesheni zake kubwa.  

Katika hali ambayo ni zaidi ya miaka mitatu sasa tangu kuanzishwa vita vya kivamizi huko Yemen, kuzinduliwa kikosi hicho cha  makombora yanayorushwa kutokea chini ya ardhi ni mafanikio makubwa ambayo yameziacha na bumbuwazi nchi vamizi. Uzinduzi huo umefanyika lengo likiwa ni kuimarisha machaguo na kuzidisha oparesheni dhidi ya muungano vamizi wa Saudi Arabia. Aidha hatua hiyo imetekelezwa katika kuimarisha uwezo wa makombora na kuzidisha kiwango cha utendaji katika uwanja wa mapambano; huku kugonga mwamba kwa nchi vamizi kukizidi kubainika wazi kufuatia kufichuliwa madai yasiyo na msingi kuhusu kusambaratishwa maeneo hayo ya kurushia  makombora ya balistiki. Katika muda wa miaka mitatu iliyopita pia kamandi za makombora za jeshi la Yemen zimefanikiwa mara kadhaa na katika minasaba tofauti kuyashambulia kwa makombora ya balistiki maeneo nyeti sana na ya kistratejia ya nchi vamizi na vibaraka wao moja baada ya jingine. 

Kombora la balistiki la Yemen baada ya kuvurumishwa kuelekea ngome ya nchi vamizi  Saudia 

Kwa msingi huo utumiaji wa maeneo hayo ya chini ya ardhi ya kurushia makombora utazidisha uwezo wa makombora wa vikosi vya Yemen na vile vile uwezo wa kujilinda. Mashambulio ya vikosi vya makombora vya Yemen dhidi ya kambi za kijeshi na za kistratejia za Saudi Arabia yamedhihirisha pia utendaji usio na ufanisi wa silaha za Marekani zilizouziwa Riyadh kama vile ngao ya makombora ya Patriot. Kuzinduliwa maeneo hayo ya kurushia makombora yaliyoko chini ya ardhi kumehitimisha njozi za viongozi wa Saudia na waitifaki wao kuwa wameharibu na kupunguza pakubwa akiba ya makombora ya vikosi vya Yemen. Kwa mafanikio hayo mapya na ya thamani  ambayo yamepatika katika mwaka wa nne wa vita hivyo vya kichokozi dhidi ya Yemen, vikosi vya nchi hiyo vimethibitisha kuwa havikabiliwi na pingamizi wala matatizo yoyote katika mashambulizi yake ya makombora dhidi ya ngome za Saudi Arabia na kwamba wanamuqawama wa Yemen wapo tayari kuendeleza oparesheni zao dhidi ya wavamizi.  Katika mazingira hayo, hakuna njia nyingine mbadala kwa muungano vamizi wa Saudia ghairi ya kukubali kushindwa huko Yemen. Hatua ya Yemen ya kutangaza kuwa ipo tayari kutekeleza mashambulizi zaidi dhidi ya nchi vamizi katika mwaka wa nne ambapo Saudi Arabia inaendesha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo jirani ni ishara kwamba Yemen bado iko imara na ina mkakati maalumu wa kukabiliana na wavamizi wa Saudi Arabia.