HAMAS: Hatujafanya mazungumzo na yeyote kuhusu "Muamala wa Karne"
(last modified Tue, 10 Jul 2018 02:24:54 GMT )
Jul 10, 2018 02:24 UTC
  • HAMAS: Hatujafanya mazungumzo na yeyote kuhusu

Mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amekanusha vikali baadhi ya madai kuhusiana na kukubali kujadili viongozi wa harakati hiyo mpango wa "Muamala wa Karne".

Ismail Ridhwan amesema wazi kuwa, madai hayo hayana ukweli wowote na kwamba, taifa la Palestina litaukwamisha mpango huo wa Marekani uliojaa njama dhidi ya taifa madhulumu la Palestina.

Baadhi ya duru za Kizayuni na za Kimagharibi hivi karibuni zilidai kuwa, viongozi wa Hamas wamefanya mazungumzo kuhusiana na vipengee vya mpango huo wa Makubaliano ya Karne.

Afisa huyo wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kwamba, mpango huo katu haukubaliki na hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika au yatakayofanyika kwa ajili ya kuujadili.

Mpango wa Rais Donald Trump wa "Muamala wa Karne" umeendelea kulaaniwa na kupingwa na Wapalestina

Hivi karibuni pia, Dakta Mahmoud al-Zahar, mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) alisisitiza kuwa, hakuna kitu kinachojulikana kwa jina la "Muamala wa Karne" katika fasihi ya taifa la Palestina.

Kwa mujibu wa mpango wa kinjama wa Marekani unaojulikana kama "Muamala wa Karne" mji wa Quds utakabidhiwa kwa utawala vamizi wa Israel, wakimbizi wa Kipalestina hawatakuwa na haki ya kurejea kwao na Wapalestina watakuwa na haki ya kumiliki sehemu ndogo tu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza.

Tags