Shehena ya mabomu ya Israel yapatikana katika maficho ya ISIS, Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46858-shehena_ya_mabomu_ya_israel_yapatikana_katika_maficho_ya_isis_syria
Jeshi la Syria limegundua shehena iliyojaa mabomu yaliyotengenezwa Israel katika mkoa wa Hama, magharibi mwa nchi; huku vikosi vya serikali vikizidi kupata mafanikio na kusonga mbele katika jitihada za kuyasafisha mabaki ya wanachama wa magenge ya kigaidi na ukufurishaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2018 03:09 UTC
  • Shehena ya mabomu ya Israel yapatikana katika maficho ya ISIS, Syria

Jeshi la Syria limegundua shehena iliyojaa mabomu yaliyotengenezwa Israel katika mkoa wa Hama, magharibi mwa nchi; huku vikosi vya serikali vikizidi kupata mafanikio na kusonga mbele katika jitihada za kuyasafisha mabaki ya wanachama wa magenge ya kigaidi na ukufurishaji.

Shirika rasmi la habari la Syria SANA limetangaza kuwa, wanajeshi wa Syria wamefanikiwa kugundua silaha hizo za utawala wa Kizayuni wa Israel, zilizokuwa zikitumiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS), katika operesheni iliyofanywa jana Jumanne kaskazini mwa mkoa huo.

Duru za kijeshi zimeripoti kuwa, vikosi vya serikali vimegundua shehena hiyo kubwa ya silaha za Israel katika mji wa Aqrab, yapata kilomita 210 kaskazini mwa mji mkuu Damascus.

Inaarifiwa kuwa, mbali na mabomu, silaha nyingine za Israel zilizopatikana kwenye shehena hiyo ya magaidi ni bunduki za kisasa za rashasha, bunduki za kulenga shabaha kwa umakini, maroketi, bastola na vyombo vya mawasiliano. 

Sehemu ndogo ya silaha za Israel na UN zilizopatikana Syria

Itakumbukwa kuwa, Februari mwaka huu, shehena nyingine za silaha zenye nambari za usajili za utawala wa Kizayuni, yakiwemo maroketi, maguruneti na vifaru zilinaswa na wanajeshi wa Syria katika miji ya Bukamal na Mayadin.

Tangu ulipoanzishwa mgogoro wa Syria mwaka 2011, utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani zimekuwa zikiwasaidia kwa hali na mali magaidi wanaofanya jinai za kutisha katika nchi hiyo ya Kiarabu.