Mashia waliozingirwa na magaidi wakufurishaji Syria kuokolewa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46860-mashia_waliozingirwa_na_magaidi_wakufurishaji_syria_kuokolewa
Mabasi kadhaa yamefika katika miji ya Kefraya na al-Foua katika mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa Syria kwa lengo la kuwahamisha Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji hiyo ambao kwa miaka kadhaa sasa wamezingirwa na magaidi wakufurishaji wanaopata himaya ya nchi za kigeni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 18, 2018 08:29 UTC
  • Mashia waliozingirwa na magaidi wakufurishaji Syria kuokolewa

Mabasi kadhaa yamefika katika miji ya Kefraya na al-Foua katika mkoa wa Idlib kaskazini magharibi mwa Syria kwa lengo la kuwahamisha Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji hiyo ambao kwa miaka kadhaa sasa wamezingirwa na magaidi wakufurishaji wanaopata himaya ya nchi za kigeni.

Televisheni ya Syria imeripoti leo Jumatano kuwa mabasi 88 yanafanya oparesheni ya kuwahamisha raia wa miji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia ya Kefraya na Al Foua ambayo inazingirwa na magaidi tokea Machi 2015.  Raia hao wapatano 6,300 wanahamishwa kutoka miji hiyo kufuatia mapatano yaliyofikiwa.

Taarifa zinasema Iran imefanya mazungumzo na wawakilishi wa kundi la kigaidi la Hay-at Tahir al Sham na kundi hilo limeafiki kuwa raia wote wataondolewa katika miji hiyo ya Kefraya na al-Foua.

Serikali ya Syria na waitifaki wake kwa kawaida hufanya mazungumzo na makundi hasimu ya kigaidi na kufikia mapatano kama hayo kwa lengo la kupunguza vifo vya raia katika oparesheni za kijeshi.

Mwaka 2017, maelfu ya raia wengine wa Kefraya na al-Foua waliondolewa katika miji hiyo na kupelekwa katika maeneo salama lakini waliosalia hawakuweza kuondolewa katika mapatano hayo.

Tokea mwaka 2011, Syria imekuwa ikikabiliana na mashambulizi ya makundi ya magaidi wakufurishaji na wanamgambo wanaopata himaya ya kigeni, hasa Marekani na Saudi Arabia. Katika miezi ya hivi karibuni, jeshi la Syria, likipata msaada wa waitifaki wake, limefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa magaidi nchini humo.