Askari wa Marekani waigeuza shule kuwa jela ya kuogofya nchini Syria
Askari vamizi wa Marekani wamegeuza jengo la shule moja huko katika mji wa Raqqa kuwa jela ya kuogofya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, jela hiyo ya kuogofya imeundwa katika jengo la shule ya kale katika mji mdogo wa Ain Isa, kaskazini mwa mji wa Raqqa ambapo imefanywa kuwa jela kubwa ambayo ndani yake wanazuiliwa maelfu ya watu. Shirika la Habari la Anatolia la nchini Uturuki, limeripoti kwamba, wafanyakazi wote wa jela hiyo, ni Wamarekani ambao wanaendesha shughuli zao kwa uficho. Aidha limeongeza kwamba askari wa Marekani wamefunga kamera kadhaa za CCTV kwenye jela hiyo yenye upana unaokaribia mita elfu 30.
Mji wa Raqqa, ambao ndio makao makuu ya jimbo la al-Raqqa, ulidhibitiwa na wanachama wa genge la kigaidi la Daesh mwaka 2013, huku ukiondoka mikononi mwa wanachama wa kundi hilo tarehe 17 Oktoba 2017 na kuingia mikononi mwa wapiganaji wa kundi la Kidemokrasia la Syria yaani 'Syrian Democratic Forces' ambalo linapata uungaji mkono kamili wa Marekani. Mgogoro wa Syria uliibuka mwaka 2011 baada ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Saudia, Marekani, Israel na waitifaki wao, kutumwa katika nchi hiyo ya Kiarabu kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali halali ya Damascus, chini ya uongozi wa Rais Bashar al-Assad. Lengo kuu la njama hizo lilikuwa ni kuleta mlingano katika eneo la Mashariki ya Kati kwa maslahi ya utawala haramu wa Kizayuni, njama ambazo hata hivyo zimeshindwa kufikia malengo yake.