Hizbullah: Ushirikiano wetu na Syria upo imara na utaendelea
Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah nchini Lebanon amesisitiza kwamba, Syria iko katika kambi ya mapambano na muqawama na kwamba uhusiano wa harakati hiyo na serikali ya Damascus upo imara na utaendelea.
Sheikh Naim Qassem ameyasema hayo alipokutana na baadhi ya wanamapambano wa Hizbullah waliokuwa wamezingirwa kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu na magaidi katika maeneo ya Waislamu wa Shia ya Al-Fu'ah na Kafriya nchini Syria, baada ya maeneo hayo kukombolewa na jeshi la nchi hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amepongeza mapambano ya wanamuqawama hao na wakazi wa maeneo hayo dhidi ya magaidi wakufurishaji na wanaosaidiwa na Marekani, Israel na Saudia mapambano ambayo hatimaye yamepelekea ushindi wa hivi karibuni.
Amesema kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya Al-Fu'ah na Kafriya hayana ukomo na ni ushindi dhidi ya njama chafu za maadui za kutaka kuibua mzozo mpya nchini Syria. Sheikh Naim Qassem amesisitiza kwamba Syria ya leo inazidi kusonga mbele na kwamba maeneo yaliyosalia chini ya udhibiti wa magaidi wanaoungwa mkono na madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu, yatakombolewa.
Katika sehemu nyingine Sheikh Naim Qassem amezungumzia azma ya kuhuishwa uhusiano kati ya Lebanon na Syria na kusema, uchumi wa Lebanon hauwezi kustafidi na uchumi wa Syria bila kufikiwa makubaliano kati ya nchi mbili. Amesema kuwa, baadhi ya watu wachache ambao wanafanya juhudi za kuzuia mahusiano kati ya Bairut na Damascus wanatumikia maslahi ya mataifa mengine; kwa sababu hiyo kuna udharura wa kuwepo mshikamano baina ya Syria na Lebanon.