Msemaji wa Ansarullah ya Yemen: UAE ni kibaraka wa Marekani
Msemaji wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: Bila Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) si lolote si chochote na ni dhaifu mno kuweza hata kupigana vita na kijiji kimoja cha Yemen.
Muhammad Abdussalam ameandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter akimhutubu Anwar Gargash, waziri mshauri katika mambo ya nje ya Imarati (UAE) kwa kusema: vita hivi vya kichokozi vimedhihirisha yale yaliyotaka kufichwa. Nyinyi Waimarati si lolote si chochote bila Marekani.
Abdussalam amesisitiza kuwa, uhusiano wa Marekani na Imarati ni wa baina ya mkoloni na mmoja wa vibaraka wa eneo.
Wakati huohuo, ripoti nyingine kutoka Yemen zinaeleza kuwa wakazi wa eneo la Sahaar na maafisa kadhaa wa mkoa wa Sa'dah leo asubuhi wameandamana kulalamikia mashambulio ya Saudi Arabia na Marekani na jinai wanazoendelea kufanya mtawalia dhidi ya wananchi wa Yemen. Waandamanaji hao wamesisitiza kuwa wataendelea kukabiliana na wavamizi hao.
Watu wasiojulikana wenye silaha wamemuua kwa kumpiga risasi Nasir Muqrih, mkuu wa usalama na intelijinsia wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden kusini mwa Yemen. Muqrih aliuawa wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwake.
Katika siku za karibuni, Aden na mikoa mingine ya kusini mwa Yemen inayokaliwa kwa mabavu na Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu, imekuwa ikishuhudia mashambulio mbalimbali ya kigaidi yanayotokana na uwepo wa makundi ya kigaidi na kukosekana amani katika maeneo hayo.../