Hasara ya dola bilioni 400 iliyosababishwa na magaidi nchini Syria
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, hasara iliyosababishwa na vita vya zaidi ya miaka saba sasa nchini Syria ni karibu dola bilioni 400.
Tathimni hiyo imetangazwa mwishoni mwa kikao cha wataalamu zaidi ya 50 wa Syria na wa kimataifa waliokutana kwa mwaliko wa Kamisheni ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa inayohusiana na masuala ya magharibi mwa Asia. Umoja wa Mataifa umesema kuwa tathmini hiyo haikujumisha idadi ya watu waliouawa, waliojeruhiwa, waliokuwa wakimbizi na waliopata madhara mengine kutokana na vita hivyo. Zaidi ya nusu ya wananchi wa Syria wamekuwa wakimbizi tangu vilipoanza vita hivyo miaka saba iliyopita na zaidi ya watu laki tatu na 50 elfu wameshauawa. Vita vya kivamizi vilivyoanzishwa na magaidi nchini Syria vimeharibu makazi ya watu, barabara, vituo vya matibabu, vituo vya mafunzo, mashule, ofisi za serikali na sehemu kubwa ya miundombinu ya Syria.
Tunapoutupia jicho mgogoro wa Syria itatubainikia kuwa baadhi ya tawala za nchi za Magharibi kwa kushirikiana na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu zilitumia vibaya cheche ya baadhi ya wananchi wa nchi hiyo kutaka marekebisho. Madola hayo na Magharibi na watawala hao madikteta wa nchi za Kiarabu walitumia fursa hiyo kumimina maelfu ya magaidi ndani ya ardhi ya Syria na kuwasha moto mkubwa ambao haujazima hadi leo hii. Magaidi waliofadhiliwa na madola ya Magharibi walianza kushambulia wananchi na maafisa wa serikali huku vyombo vya habari vya Magharibi vikafunga kibwebwe cha kupotosha ukweli kuhusu jinai za magaidi hao. Madola hayo ya Magharibi yalidai kuwa eti ni serikali ya Syria ndiyo iliyokuwa inaua wananchi wake na eti ni wananchi ndio waliokuwa wanapigana na maafisa usalama wa serikali. Mashambulizi ya magaidi wanaoungwa mkono na madola ya Magharibi huko Syria yameharibu sehemu kubwa ya sekta ya kilimo ya nchi hiyo. Sekta ya utalii ya Syria nayo ambayo ilikuwa ni moja ya vyanzo muhimu vya pato la nchi hiyo imeharibiwa kikamilifu na vita hivyo.
Bouthaina Shaaban, mshauri wa kisiasa na masuala ya vyombo vya habari wa Rais Bashar al Assad wa Syria amesema kuwa kiwango kukubwa cha uharibifu ndani ya Syria uliofanywa kwa njama za nchi za Magharibi unaonesha kuwa Marekani na vitimbakwiri vyake wamemiminika nchini Syria kwa lengo la kuharibu miundombinu ya kiuchumi, kisiasa na ustaarabu mkongwe wa nchi hiyo.
Kiwango kikubwa cha uharibifu unaofanywa na ndege za kivita za Marekani katika nchi za Iraq na Syria kwa madai ya kupambana na ugaidi ambapo badala ya kuwashambulia magaidi, ndege hizo zinashambulia miundombinu ya nchi hiyo, ni ushahidi mwingine wa wazi wa njama kubwa za madola ya Magharibi za kuangamiza kikamilifu uwezo wa kiuchumi na kimaendeleo wa nchi hizo. Vita vya magaidi dhidi ya taifa la Syria vimeisababishia hasara kubwa nchi hiyo ya Kiarabu kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ikiwa ni pamoja na hatari zinazotokana na kuendelea vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi dhidi ya Syria. Naam lengo la kuendelezwa vikwazo vya kiuchumi vya nchi za Magharibi dhidi ya Syria sambamba na mashambulizi ya magaidi wanaoungwa mkono kwa kila hali na Wamagharibi, ni kuvuruga njia zote za kufufuka kiuchumi nchi hiyo. Vikwazo vya kiuchumi vya Magharibi dhidi ya wananchi wa Syria vinaendelea katika hali ambayo nchi za Marekani, Uingereza na Ufaransa huwa zinaitisha vikao vya eti marafiki wa Syria na kujifanya zinawaonea huruma sana wananchi wa nchi hiyo. Kwa kweli jinai zinazoendelea kufanywa na magaidi huko Syria kwa uungaji mkono kamili wa madola ya Magharibi zimeifanya nchi hiyo kukubwa na migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu katika zama hizi na hicho ndicho kitu kilichoashiriwa katika ripoti ya hivi sasa ya Umoja wa Mataifa.